| ← 2Corinthians (8/13) → |
| 1. | Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; |
| 2. | maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. |
| 3. | Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; |
| 4. | wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. |
| 5. | Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu. |
| 6. | Hata tukamwonya Tito kuwatimilizia neema hii kwenu kama vile yeye alivyotangulia kuianzisha. |
| 7. | Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia. |
| 8. | Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu. |
| 9. | Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. |
| 10. | Nami katika neno hili natoa shauri langu; maana neno hili lawafaa ninyi mliotangulia, yapata mwaka, licha ya kutenda hata na kutaka pia. |
| 11. | Lakini sasa timizeni kule kutenda nako, ili kama vile mlivyokuwa tayari kutaka, vivyo hivyo mkawe tayari na kutimiza, kwa kadiri ya mlivyo navyo. |
| 12. | Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo. |
| 13. | Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki; |
| 14. | bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa. |
| 15. | Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa. |
| 16. | Lakini ahimidiwe Mungu atiaye bidii ile ile kwa ajili yenu katika moyo wa Tito. |
| 17. | Maana aliyapokea kweli yale maonyo; tena, huku akizidi kuwa na bidii, alisafiri kwenda kwenu kwa hiari yake mwenyewe. |
| 18. | Na pamoja naye tukamtuma ndugu yule ambaye sifa zake katika Injili zimeenea makanisani mwote. |
| 19. | Wala si hivyo tu, bali alichaguliwa na makanisa asafiri pamoja nasi katika jambo la neema hii, tunayoitumikia, ili Bwana atukuzwe, ukadhihirike utayari wetu. |
| 20. | Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii tunayoitumikia; |
| 21. | tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu. |
| 22. | Nasi pamoja nao tumemtuma ndugu yetu tuliyemwona mara nyingi katika mambo mengi kuwa ana bidii, na sasa ana bidii zaidi sana kwa sababu ya tumaini kuu alilo nalo kwenu. |
| 23. | Basi mtu akitaka habari za Tito, yeye ni mshirika wangu, na mtenda kazi pamoja nami kwa ajili yenu; tena akitaka habari za ndugu zetu, wao ni mitume wa makanisa, na utukufu wa Kristo. |
| 24. | Basi waonyesheni mbele ya makanisa hakika ya upendo wenu, na ya kujisifu kwetu kwa ajili yenu. |
| ← 2Corinthians (8/13) → |