| ← 2Corinthians (12/13) → |
| 1. | Sina budi kujisifu, ijapokuwa haipendezi; lakini nitafikilia maono na mafunuo ya Bwana. |
| 2. | Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. |
| 3. | Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); |
| 4. | ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene. |
| 5. | Kwa habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu. |
| 6. | Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu. |
| 7. | Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. |
| 8. | Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. |
| 9. | Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. |
| 10. | Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu. |
| 11. | Nimekuwa mpumbavu, ninyi mmenilazimisha. Maana ilinipasa nisifiwe na ninyi; kwa sababu sikuwa duni ya mitume walio wakuu kwa lo lote, nijapokuwa si kitu. |
| 12. | Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika saburi yote, kwa ishara na maajabu na miujiza. |
| 13. | Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe udhalimu huu. |
| 14. | Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto. |
| 15. | Nami kwa furaha nyingi nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa? |
| 16. | Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu naliwapata kwa hila. |
| 17. | Je! Mtu ye yote niliyemtuma kwenu, kwa mtu huyo naliwatoza kitu? |
| 18. | Nalimwonya Tito, nikamtuma ndugu yule pamoja naye. Je! Tito aliwatoza kitu? Je! Hatukuenenda kwa Roho yeye yule na katika nyayo zile zile? |
| 19. | Mwadhani hata sasa ya kuwa najidhuru kwenu! Mbele za Mungu twanena katika Kristo. Na hayo yote, wapenzi, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi. |
| 20. | Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong'onezo, na majivuno, na ghasia; |
| 21. | nami nitakapokuja tena, Mungu wangu asije akanidhili kwenu, nami nikawasikitikia wengi waliokosa tangu hapo, wasiutubie uchafu, na uasherati, na ufisadi walioufanya. |
| ← 2Corinthians (12/13) → |