← 2Corinthians (11/13) → |
1. | Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami. |
2. | Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. |
3. | Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. |
4. | Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye! |
5. | Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu. |
6. | Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu. |
7. | Je! Nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira? |
8. | Naliwanyang'anya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu ili niwahudumie ninyi. |
9. | Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote najilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena najilinda. |
10. | Kama vile ile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu atakayenifumba kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya. |
11. | Kwa nini? Je! Ni kwa sababu siwapendi ninyi? Mungu anajua. |
12. | Lakini nifanyalo nitalifanya, ili niwapinge hao watafutao nafasi wasipate nafasi; ili kwamba katika neno hilo wajisifialo waonekane kuwa kama sisi. |
13. | Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. |
14. | Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. |
15. | Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao. |
16. | Nasema tena, mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; ili mimi nami nipate kujisifu ngaa kidogo. |
17. | Ninenalo silineni agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu. |
18. | Kwa sababu wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili, mimi nami nitajisifu. |
19. | Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnachukuliana na wajinga kwa furaha. |
20. | Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni. |
21. | Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Walakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri. |
22. | Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Ibrahimu? Na mimi pia. |
23. | Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. |
24. | Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. |
25. | Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; |
26. | katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; |
27. | katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. |
28. | Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote. |
29. | Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe? |
30. | Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu. |
31. | Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo. |
32. | Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata; |
33. | nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake. |
← 2Corinthians (11/13) → |