2Corinthians (10/13)  

1. Basi, mimi Paulo mwenyewe nawasihi kwa upole na utaratibu wa Kristo; mimi niliye mnyenyekevu nikiwapo pamoja nanyi, bali nisipokuwapo ni mwenye ujasiri kwenu;
2. naam, naomba kwamba nikiwapo, nisiwe na ujasiri kwa uthabiti ambao nahesabu kuwa nao juu ya wale wanaodhania ya kuwa sisi tunaenenda kwa jinsi ya mwili.
3. Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;
4. (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)
5. tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;
6. tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.
7. Yaangalieni yaliyo mbele ya macho yenu. Mtu akijitumainia mwenyewe ya kuwa ni mtu wa Kristo, na afikiri hivi pia nafsini mwake, ya kwamba kama yeye alivyo mtu wa Kristo, vivyo hivyo na sisi.
8. Maana, nijapojisifu zaidi kidogo kwa ajili ya mamlaka yetu, (tuliyopewa na Bwana, tupate kuwajenga wala si kuwaangusha), sitatahayarika;
9. nisije nikaonekana kana kwamba nataka kuwaogofya kwa nyaraka zangu.
10. Maana wasema, Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu.
11. Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo.
12. Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili.
13. Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu.
14. Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika injili ya Kristo;
15. wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada;
16. hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa.
17. Lakini, Yeye ajisifuye, na ajisifu katika Bwana.
18. Maana mtu mwenye kukubaliwa si yeye ajisifuye, bali yeye asifiwaye na Bwana.

  2Corinthians (10/13)