← 2Chronicles (7/36) → |
1. | Basi Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba. |
2. | Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana umeijaza nyumba ya Bwana. |
3. | Wakatazama wana wa Israeli wote, uliposhuka ule moto, utukufu wa Bwana ulipokuwapo juu ya nyumba; wakasujudu kifulifuli hata nchi sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele. |
4. | Ndipo mfalme na watu wote wakatoa dhabihu mbele za Bwana. |
5. | Mfalme Sulemani akatoa sadaka ya ng'ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na watu wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Mungu. |
6. | Wakasimama makuhani sawasawa na malinzi yao; Walawi nao pamoja na vinanda vya Bwana, alivyovifanya Daudi mfalme, ili kumshukuru Bwana, kwa maana fadhili zake ni za milele, hapo aliposifu Daudi kwa mikono yao; nao makuhani wakapiga panda mbele yao; nao Israeli wote wakasimama. |
7. | Tena Sulemani akaitakasa behewa katikati, iliyokuwa mbele ya nyumba ya Bwana; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba aliyoifanya Sulemani haikutosha kuzipokea sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta. |
8. | Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba. |
9. | Hata siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana walishika kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba. |
10. | Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote Bwana aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake. |
11. | Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa Bwana, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha. |
12. | Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. |
13. | Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; |
14. | ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. |
15. | Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. |
16. | Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima. |
17. | Nawe, ukienda mbele yangu kama alivyokwenda Daudi baba yako, ufanye sawasawa na yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu; |
18. | ndipo nitakithibitisha kiti cha enzi cha ufalme wako, kama nilivyoagana na Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kutawala katika Israeli. |
19. | Lakini mkigeuka, na kuziacha sheria zangu na amri zangu nilizoweka mbele yenu, mkienda, na kuitumikia miungu mingine, na kuiabudu; |
20. | ndipo nitawang'oa katika nchi yangu niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaiondosha itoke mbele zangu, nami nitaifanya kuwa mithali na tukano katikati ya watu wote. |
21. | Na nyumba hii, iliyo juu, kila apitaye ataona ushangao, atasema, Mbona Bwana ameitendea hivi nchi hii, na nyumba hii? |
22. | Nao watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu, na kuitumikia; kwa hiyo ameyaleta mabaya haya yote juu yao. |
← 2Chronicles (7/36) → |