← 2Chronicles (35/36) → |
1. | Naye Yosia akamfanyia Bwana pasaka huko Yerusalemu; wakachinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. |
2. | Akawasimamisha makuhani katika malinzi yao, akawatia moyo kufanya utumishi wa nyumba ya Bwana. |
3. | Akawaambia Walawi, waliowafundisha Israeli wote, waliotakasika kwa Bwana, Wekeni sanduku takatifu katika nyumba aliyoijenga Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli; hamtakuwa tena na mzigo mabegani; sasa mtumikieni Bwana, Mungu wenu, na watu wake Israeli. |
4. | Mkajiweke tayari kwa kadiri ya nyumba za baba zenu, kwa zamu zenu, kama alivyoandika Daudi mfalme wa Israeli, na kama alivyoandika Sulemani mwanawe. |
5. | Mkasimame katika patakatifu, kama walivyogawanyika ndugu zenu, wana wa watu, kufuata nyumba za mababa, kadiri ya mgawanyiko wa kila nyumba ya baba, ya Walawi. |
6. | Mkachinje pasaka, mkajitakase, mkawatengenezee ndugu zenu, kutenda sawasawa na neno la Bwana kwa mkono wa Musa. |
7. | Tena Yosia akawapa wana wa watu, matoleo ya makundi, wana-kondoo na wana-mbuzi, yote yawe kwa ajili ya matoleo ya pasaka, wote waliokuwako, wakipata thelathini elfu, na ng'ombe elfu tatu; hao walitoka katika mali za mfalme. |
8. | Na wakuu wake wakawapa watu, na makuhani na Walawi matoleo ya hiari. Hilkia na wana na Yehieli, wakubwa wa nyumba ya Mungu, wakawapa makuhani, kuwa matoleo ya pasaka, wana-kondoo elfu mbili na mia sita, na ng'ombe mia tatu. |
9. | Konania naye, na Shemaya, na Nethaneli, ndugu zake, na Hashabia, na Yeieli, na Yozabadi, wakuu wa Walawi, wakawapa Walawi, kuwa matoleo ya pasaka, wana-kondoo elfu tano, na ng'ombe mia tano. |
10. | Hivyo huduma ikatengenezwa, wakasimama makuhani mahali pao, na Walawi kwa zamu zao, kama alivyoamuru mfalme. |
11. | Wakachinja pasaka, nao makuhani wakamimina damu waliyopokea mikononi mwao, Walawi wakachuna. |
12. | Wakaziondoa sadaka za kuteketezwa, wawape wana wa watu, kama walivyogawanyika kufuata nyumba za mababa, ili wamtolee Bwana, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Musa. Nao ng'ombe wakawafanya vivyo hivyo. |
13. | Wakaioka moto pasaka kama ilivyo sheria; wakatokosa matoleo matakatifu vyunguni, na masufuriani, na makaangoni, wakawachukulia upesi wana wa watu wote. |
14. | Baadaye wakajiandalia wenyewe, na makuhani; kwa sababu makuhani, wana wa Haruni, walikuwa na kazi ya kutoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta hata usiku; kwa hiyo Walawi wakajiandalia wenyewe, na makuhani, wana wa Haruni. |
15. | Nao waimbaji, wana wa Asafu wakasimama mahali pao, kama alivyoamuru Daudi, na Asafu, na Hemani, na Yeduthuni mwonaji wa mfalme; nao mabawabu walikuwa katika kila lango; hawakuhitaji kuondoka katika huduma yao, kwa kuwa ndugu zao Walawi wakawaandalia. |
16. | Basi huduma yote ya Bwana ikatengenezwa siku ile ile, kuifanya pasaka, na kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana, kama alivyoamuru mfalme Yosia. |
17. | Wana wa Israeli waliokuwapo wakafanya pasaka wakati ule, na sikukuu ya mikate isiyochachwa muda wa siku saba. |
18. | Wala haikufanyika pasaka kama ile katika Israeli tangu siku za nabii Samweli; wala wafalme wa Israeli hawakufanya hata mmoja wao pasaka kama ile Yosia aliyoifanya, pamoja na makuhani, na Walawi, na Yuda wote na Israeli waliokuwapo, na wenyeji wa Yerusalemu. |
19. | Katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake Yosia ikafanyika pasaka hiyo. |
20. | Baada ya hayo yote, alipokwisha Yosia kulitengeneza hekalu, Neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana Karkemishi karibu na Frati; naye Yosia akatoka juu yake. |
21. | Lakini yeye akatuma kwake wajumbe, kusema, Ni nini niliyo nayo mimi na wewe, Ee mfalme wa Yuda? Sikuja juu yako leo, lakini juu ya nyumba niliyo na vita nayo; naye Mungu ameniamuru nifanye haraka; acha basi kumpinga Mungu, aliye pamoja nami, asikuharibu. |
22. | Walakini Yosia hakukubali kumgeuzia uso mbali, akajibadilisha apate kupigana naye, asiyasikilize maneno ya Neko, yaliyotoka kinywani kwa Mungu, akaja kupigana bondeni mwa Megido. |
23. | Nao wapiga upinde wakampiga Yosia; naye mfalme akawaambia watumishi wake, Niondoeni; kwani nimejeruhiwa sana. |
24. | Basi watumishi wake wakamtoa garini, wakamtia katika gari la pili alilokuwa nalo, wakamleta Yerusalemu; naye akafa, akazikwa makaburini mwa babaze. Wakamlilia Yosia Yuda wote na Yerusalemu. |
25. | Naye Yeremia akamlilia Yosia; na waimbaji wote waume kwa wake wakamtaja Yosia katika maombolezo yao, hata leo; hata wakayafanya kuwa ada kwa Israeli; nayo, tazama, yameandikwa katika maombolezo. |
26. | Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na matendo yake mema, sawasawa na yote yaliyoandikwa katika torati ya Bwana, |
27. | na mambo yake, ya kwanza na ya mwisho, tazama, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda. |
← 2Chronicles (35/36) → |