← 2Chronicles (20/36) → |
1. | Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, |
2. | Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi). |
3. | Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute Bwana; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. |
4. | Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute Bwana; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta Bwana. |
5. | Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa Bwana, mbele ya ua mpya; |
6. | akasema, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako. |
7. | Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Ibrahimu rafiki yako hata milele? |
8. | Nao walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema, |
9. | Yakitujia mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida yetu, nawe utasikia na kuokoa. |
10. | Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu; |
11. | tazama, jinsi wanavyotulipa, wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha. |
12. | Ee Mungu wetu, je! Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yatazama kwako. |
13. | Wakasimama Yuda wote mbele za Bwana, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao. |
14. | Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya Bwana, katikati ya kusanyiko; |
15. | akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; Bwana awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. |
16. | Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli. |
17. | Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa Bwana ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa Bwana yu pamoja nanyi. |
18. | Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za Bwana Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia Bwana. |
19. | Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. |
20. | Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. |
21. | Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia Bwana, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni Bwana; kwa maana fadhili zake ni za milele. |
22. | Nao walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. |
23. | Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. |
24. | Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. |
25. | Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana. |
26. | Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipombarikia Bwana; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo. |
27. | Kisha wakarudi, kila mtu wa Yuda na Yerusalemu, na Yehoshafati mbele yao, ili kuurudia Yerusalemu kwa furaha; kwa kuwa Bwana amewafurahisha juu ya adui zao. |
28. | Wakafika Yerusalemu wenye vinanda vinubi na mapanda kwenda nyumbani kwa Bwana. |
29. | Ikawa hofu ya Mungu juu ya falme zote za nchi, waliposikia ya kuwa Bwana amepigana juu ya adui za Israeli. |
30. | Basi ukatulia ufalme wake Yehoshafati; kwa sababu Mungu wake alimstarehesha pande zote. |
31. | Yehoshafati akatawala juu ya Yuda; alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala, akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi. |
32. | Akaiendea njia ya Asa babaye, wala hakuiacha, akifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. |
33. | Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; wala mioyo ya watu bado haijakazwa kwa Mungu wa baba zao. |
34. | Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, ya kwanza na ya mwisho, angalia, yameandikwa katika tarehe ya Yehu mwana wa Hanani, iliyotiwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli. |
35. | Baada ya hayo Yehoshafati mfalme wa Yuda akapatana na Ahazia mfalme wa Israeli; naye huyo ndiye aliyefanya mabaya mno; |
36. | akapatana naye kufanya merikebu za kuendea Tarshishi; wakazifanya merikebu zile huko Esion-geberi. |
37. | Ndipo Eliezeri mwana wa Dodavahu wa Maresha akatoa unabii juu ya Yehoshafati, akasema, Kwa sababu umepatana na Ahazia, Bwana amezivunja-vunja kazi zako. Zikavunjika merikebu, zisiweze kufika Tarshishi. |
← 2Chronicles (20/36) → |