| ← 2Chronicles (18/36) → |
| 1. | Basi, Yehoshafati alikuwa na mali na heshima tele, tena akafanya ujamaa na Ahabu. |
| 2. | Hata baada ya miaka kadha wa kadha akamshukia Ahabu huko Samaria. Ahabu akamchinjia kondoo na ng'ombe tele, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, akamshawishi ili apande pamoja naye waende Ramoth-gileadi. |
| 3. | Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwambia Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Je! Utakwenda nami mpaka Ramoth-gileadi? Akamjibu, Mimi ni kama wewe, na watu wangu kama watu wako; nasi tutakuwa pamoja nawe vitani. |
| 4. | Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana. |
| 5. | Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya manabii, watu mia nne; akawaambia, Je! Tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Wakasema, Kwea; kwa kuwa Mungu atautia mkononi mwa mfalme. |
| 6. | Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa Bwana tena, ili tumwulize yeye? |
| 7. | Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema kamwe, ila siku zote mabaya; naye ndiye Mikaya mwana wa Imla. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. |
| 8. | Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida mmoja, akasema, Mlete hima Mikaya mwana wa Imla. |
| 9. | Basi, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wamekaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, wakikaa penye sakafu pa kuingilia lango la Samaria; nao manabii wote wakafanya unabii mbele yao. |
| 10. | Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, Bwana asema hivi, Kwa hizi utawasukuma Washami, hata watakapoangamia. |
| 11. | Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme. |
| 12. | Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema. |
| 13. | Mikaya akasema, Kama aishivyo Bwana, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena. |
| 14. | Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu. |
| 15. | Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana? |
| 16. | Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. |
| 17. | Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya? |
| 18. | Mikaya akasema, Sikieni basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto. |
| 19. | Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. |
| 20. | Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani? |
| 21. | Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo. |
| 22. | Basi sasa, angalia, Bwana ametia pepo wa uongo vinywani mwa manabii wako hawa; naye Bwana amenena mabaya juu yako. |
| 23. | Ndipo akakaribia Zedekia mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Alitokaje kwangu roho ya Bwana ili aseme na wewe? |
| 24. | Mikaya akasema, Angalia utaona siku ile, utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche. |
| 25. | Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme; |
| 26. | mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani. |
| 27. | Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, Bwana hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote. |
| 28. | Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-gileadi. |
| 29. | Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha; nao wakaingia vitani. |
| 30. | Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru maakida wa magari yake, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake. |
| 31. | Ikawa maakida wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Mfalme wa Israeli ni huyu. Basi wakamgeukia ili wapigane naye; lakini Yehoshafati akalia, na Bwana akamsaidia; Mungu akawafarakisha kwake. |
| 32. | Ikawa, maakida wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate. |
| 33. | Na mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana. |
| 34. | Pigano likazidi siku ile; lakini mfalme wa Israeli akajitegemeza garini juu ya Washami hata jioni; akafa kama wakati wa kuchwa kwa jua. |
| ← 2Chronicles (18/36) → |