| ← 2Chronicles (14/36) → | 
| 1. | Basi Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi, akatawala Asa mwanawe mahali pake; katika siku zake nchi ikastarehe miaka kumi. | 
| 2. | Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa Bwana, Mungu wake; | 
| 3. | maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera; | 
| 4. | akawaamuru Yuda wamtafute Bwana, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri. | 
| 5. | Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake. | 
| 6. | Akajenga miji yenye maboma katika Yuda; kwa kuwa nchi ilikuwa imestarehe, wala hakuwa na vita miaka ile; kwa sababu Bwana amemstarehesha. | 
| 7. | Naye akawaambia Yuda, Na tuijenge miji hii, na kuizungushia maboma, na minara, na malango, na makomeo; nchi bado ikalipo mbele yetu, kwa kuwa tumemtafuta Bwana, Mungu wetu; naam, tumemtafuta, naye amemstarehesha pande zote. Basi wakajenga, wakafanikiwa. | 
| 8. | Naye Asa alikuwa na jeshi waliochukua ngao na mikuki, katika Yuda mia tatu elfu; na katika Benyamini wenye kuchukua vigao na kupinda upinde, mia mbili na themanini elfu; hao wote walikuwa mashujaa. | 
| 9. | Kisha, akatoka juu yao Zera Mkushi, mwenye jeshi elfu elfu, na magari mia tatu; akaja Maresha. | 
| 10. | Akatoka Asa amlaki, wakapanga vita Maresha bondeni mwa Sefatha. | 
| 11. | Naye Asa akamlilia Bwana, Mungu wake, akasema, Bwana, hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake yeye aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidie, Ee Bwana, Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu. | 
| 12. | Basi, Bwana akawapiga Wakushi mbele ya Asa, na mbele ya Yuda; na Wakushi wakakimbia. | 
| 13. | Asa na watu waliokuwa pamoja naye wakawafuata mpaka Gerari; nao wengi wakaanguka wa Wakushi hata wasiweze kupona; kwa sababu waliangamizwa mbele za Bwana, na mbele ya jeshi lake; na hao wakachukua mateka mengi sana. | 
| 14. | Wakaipiga miji yote kando-kando ya Gerari; maana hofu ya Bwana ikawajia; nao wakaiteka nyara miji yote, kwa maana zilikuwamo ndani yake nyara nyingi mno. | 
| 15. | Wakazipiga pia hema za ng'ombe, wakachukua kondoo wengi na ngamia, wakarudi Yerusalemu. | 
| ← 2Chronicles (14/36) → |