← 2Chronicles (13/36) → |
1. | Katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu, akaanza Abiya kutawala juu ya Yuda. |
2. | Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka binti Urieli wa Gibea. Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu. |
3. | Abiya akapanga vita mwenye jeshi la watu hodari wa vita, watu wateule mia nne elfu; naye Yeroboamu akapanga vita juu yake mwenye watu wateule mia nane elfu, waliokuwa waume mashujaa. |
4. | Basi Abiya akasimama juu ya kilima cha Semaraimu, kilichoko milimani mwa Efraimu, akasema, Nisikieni, enyi Yeroboamu na Israeli wote; |
5. | je! Haikuwapasa kujua ya kwamba Bwana, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi? |
6. | Lakini Yeroboamu mwana wa Nebati, mtumwa wa Sulemani mwana wa Daudi, akainuka, akamfanyia fitina bwana wake. |
7. | Wakamkusanyikia watu mabaradhuli, wasiofaa kitu, waliojitia nguvu juu ya Rehoboamu mwana wa Sulemani, Rehoboamu alipokuwa kijana na wa moyo mwororo, asiweze kuwazuia. |
8. | Hata sasa mwajidhania kuwa mtauzuia ufalme wa Bwana mikononi mwa wana wa Daudi; nanyi mmekuwa jamii kubwa, na kwenu mna ndama za dhahabu alizowafanyia Yeroboamu kuwa miungu. |
9. | Je! Hamkuwafukuza makuhani wa Bwana, wana wa Haruni, na Walawi; mkajifanyia makuhani kama wafanyavyo watu wa nchi nyingine? Hata ye yote ajaye kujifanya wakfu na ndama, na kondoo waume saba, aweza kuwa kuhani wa hiyo isiyo miungu. |
10. | Lakini sisi, Bwana ndiye Mungu wetu, wala sisi hatukumwacha; tena tunao makuhani wanaomtumikia Bwana, wana wa Haruni, na Walawi, kwa kazi yao; |
11. | nao humtolea Bwana kila asubuhi, na kila jioni, sadaka za kuteketezwa na fukizo la manukato; mikate ya wonyesho pia huiweka kwa taratibu yake juu ya meza takatifu, na kinara cha dhahabu chenye taa zake, kuwaka kila jioni; kwa maana sisi twayalinda malinzi ya Bwana, Mungu wetu; bali ninyi mmemwacha. |
12. | Na tazama, Mungu yu pamoja nasi atutangulie, na makuhani wake wenye mapanda, ili wapige sauti ya kugutusha juu yenu. Enyi wana wa Israeli, msipigane na Bwana, Mungu wa baba zenu; kwani hamtafanikiwa. |
13. | Lakini Yeroboamu aliwazungushia waviziao kwa nyuma; basi wao wakawa mbele ya Yuda, na wale waviziao nyuma yao. |
14. | Na Yuda walipotazama nyuma, angalia, vita vikawa mbele na nyuma; wakamlilia Bwana, na makuhani wakapiga mapanda. |
15. | Ndipo wakapiga kelele watu wa Yuda; ikawa, watu na Yuda walipopiga kelele, Mungu akampiga Yeroboamu na Israeli wote mbele ya Abiya na Yuda. |
16. | Wana wa Israeli wakakimbia mbele ya Yuda; naye Mungu akawaua mikononi mwao. |
17. | Abiya na watu wake wakawapiga mapigo makuu; hata wakaanguka wameuawa wa Israeli mia tano elfu, watu wateule. |
18. | Ndivyo walivyotiishwa wana wa Israeli wakati ule, wakashinda wana wa Yuda, kwa kuwa walimtegemea Bwana, Mungu wa baba zao. |
19. | Abiya akamfuata Yeroboamu, akamnyang'anya miji, Betheli na miji yake, na Yeshana na miji yake, na Efroni na miji yake. |
20. | Wala Yeroboamu hakupata nguvu tena siku za Abiya; kisha Bwana akampiga, akafa. |
21. | Ila Abiya akapata nguvu, akaoa wake kumi na wanne, akazaa wana ishirini na wawili, na binti kumi na sita. |
22. | Na mambo ya Abiya yaliyosalia, na njia zake, na maneno yake, yameandikwa katika kitabu cha maelezo cha nabii Ido. |
← 2Chronicles (13/36) → |