2Chronicles (12/36)  

1. Ikawa ulipothibitika ufalme wa Rehoboamu, naye amepata nguvu, aliiacha torati ya Bwana, na Israeli wote pamoja naye.
2. Ikawa katika mwaka wa tano wa mfalme Rehoboamu, akapanda Shishaki, mfalme wa Misri, juu ya Yerusalemu; kwa kuwa walikuwa wamemwasi Bwana;
3. mwenye magari elfu moja na mia mbili, na wapanda farasi sitini elfu; na watu wasiohesabika, waliotoka Misri pamoja naye; Walubi, na Wasukii, na Wakushi.
4. Akaitwaa miji yenye maboma iliyokuwa ya Yuda, akaja Yerusalemu.
5. Ndipo akaja Shemaya nabii kwa Rehoboamu, na kwa wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu kwa sababu ya Shishaki, akawaambia, Bwana asema hivi, Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo nami nimewaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.
6. Ndipo wakajinyenyekeza wakuu wa Israeli na mfalme; wakasema, Bwana ndiye mwenye haki.
7. Naye Bwana alipoona ya kwamba wamejinyenyekeza, neno la Bwana likamjia Shemaya, kusema, Wamejinyenyekeza; sitawaharibu; lakini nitawapa wokovu punde, wala ghadhabu yangu haitamwagika juu ya Yerusalemu kwa mkono wa Shishaki.
8. Walakini watamtumikia; ili wapate kujua utumwa wangu, na huo utumwa wa falme za nchi.
9. Basi Shishaki, mfalme wa Misri, akapanda juu ya Yerusalemu, akazichukua hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme; akazichukua zote. Akazichukua pia ngao za dhahabu alizozifanya Sulemani.
10. Mfalme Rehoboamu akafanya ngao za shaba mahali pake, akawakabidhi wakuu wa walinzi, waliongoja mlangoni pa nyumba ya mfalme.
11. Ikawa kila wakati mfalme alipoingia nyumbani mwa Bwana, wakaja walinzi wakazichukua, wakazirudisha tena chumbani mwa walinzi.
12. Naye alipojinyenyekeza, ghadhabu ya Bwana ikamgeukia mbali, asimharibu kabisa; tena yalionekana katika Yuda mambo mema.
13. Basi mfalme Rehoboamu akajitia nguvu katika Yerusalemu, akatawala; maana Rehoboamu alikuwa na umri wa miaka arobaini na mmoja alipoanza kutawala, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua Bwana miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke huko jina lake. Na jina la mamaye aliitwa Naama Mwamoni.
14. Naye akatenda yaliyo maovu, kwa kuwa hakuukaza moyo wake amtafute Bwana.
15. Basi mambo yake Rehoboamu, ya kwanza na ya mwisho, je! Hayakuandikwa katika tarehe za Shemaya nabii na Ido mwonaji, kwa jinsi ya kuandika nasaba? Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote.
16. Rehoboamu akalala na babaze, akazikwa katika mji wa Daudi. Na Abiya mwanawe alitawala mahali pake.

  2Chronicles (12/36)