← 2Chronicles (10/36) → |
1. | Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekuja Shekemu, ili wamfanye mfalme. |
2. | Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia, (maana alikuwako Misri, ambako amekimbilia mbele ya mfalme Sulemani), Yeroboamu akarudi kutoka Misri. |
3. | Wakapeleka ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, |
4. | Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. |
5. | Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao. |
6. | Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa? |
7. | Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote. |
8. | Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, waliosimama mbele yake. |
9. | Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, Utufanyie jepesi kongwa alilotutwika baba yako. |
10. | Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. |
11. | Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu akiwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. |
12. | Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. |
13. | Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana, |
14. | akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. |
15. | Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Mungu, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni. |
16. | Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hawasikilizi, watu wakamjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli, kila mtu; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Daudi. Basi wakaenda zao Israeli wote hemani kwao. |
17. | Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu alitawala juu yao. |
18. | Ndipo mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, msimamizi wa shokoa; nao wana wa Israeli wakamtupia mawe, hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda garini mwake, ili akimbilie Yerusalemu. |
19. | Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi, hata leo. |
← 2Chronicles (10/36) → |