1Timothy (1/6)  

1. Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu;
2. kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
3. Kama vile nilivyokusihi ukae Efeso, nilipokuwa nikisafiri kwenda Makedonia, ili uwakataze wengine wasifundishe elimu nyingine;
4. wala wasiangalie hadithi na nasaba zisizo na ukomo, ziletazo maswali wala si madaraka ya Mungu yaliyo katika imani; basi ufanye hivyo.
5. Walakini mwisho wa agizo hilo ni upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na unafiki.
6. Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili;
7. wapenda kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo yale wayanenayo kwa uthabiti.
8. Lakini twajua ya kuwa sheria ni njema, kama mtu akiitumia kwa njia iliyo halali;
9. akilifahamu neno hili, ya kuwa sheria haimhusu mtu wa haki, bali waasi, na wasio wataratibu, na makafiri, na wenye dhambi, na wanajisi, na wasiomcha Mungu, na wapigao baba zao, na wapigao mama zao, na wauaji,
10. na wazinifu, na wafiraji, na waibao watu, na waongo, nao waapao kwa uongo; na likiwapo neno lo lote linginelo lisilopatana na mafundisho yenye uzima;
11. kama vile ilivyonenwa katika Habari Njema ya utukufu wa Mungu ahimidiwaye, niliyowekewa amana.
12. Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;
13. ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani.
14. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu.
15. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.
16. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.
17. Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.
18. Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba, kwa ajili ya maneno ya unabii yaliyotangulia juu yako, ili katika hayo uvipige vile vita vizuri;
19. uwe mwenye imani na dhamiri njema, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia kwa habari ya Imani.
20. Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

      1Timothy (1/6)