← 1Thessalonians (5/5) |
1. | Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. |
2. | Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. |
3. | Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. |
4. | Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. |
5. | Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. |
6. | Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. |
7. | Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. |
8. | Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. |
9. | Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo; |
10. | ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, kwamba twakesha au kwamba twalala. |
11. | Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya. |
12. | Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; |
13. | mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi. |
14. | Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote. |
15. | Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. |
16. | Furahini siku zote; |
17. | ombeni bila kukoma; |
18. | shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. |
19. | Msimzimishe Roho; |
20. | msitweze unabii; |
21. | jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; |
22. | jitengeni na ubaya wa kila namna. |
23. | Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. |
24. | Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya. |
25. | Ndugu, tuombeeni. |
26. | Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu. |
27. | Nawaapisha kwa Bwana, ndugu wote wasomewe waraka huu. |
28. | Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. |
← 1Thessalonians (5/5) |