| ← 1Thessalonians (3/5) → |
| 1. | Basi kwa hiyo, tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliona vema kuachwa Athene peke yetu. |
| 2. | Tukamtuma Timotheo ndugu yetu, mtumishi wa Mungu katika Injili ya Kristo, ili kuwafanya ninyi imara na kuwafariji kwa habari ya imani yenu; |
| 3. | mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo. |
| 4. | Kwa kuwa tulipokuwapo kwenu tulitangulia kuwaambia kwamba tutapata dhiki, kama ilivyotukia, nanyi mwajua. |
| 5. | Kwa hiyo mimi nami nilipokuwa siwezi kuvumilia tena, nalituma mtu ili niijue imani yenu, asije yule mjaribu akawajaribu, na taabu yetu ikawa haina faida. |
| 6. | Lakini Timotheo alipotujia hivi sasa kutoka kwenu, alituletea habari njema za imani yenu na upendo wenu, na ya kwamba mnatukumbuka vema siku zote; mkitamani kutuona sisi vile vile kama sisi kuwaona ninyi. |
| 7. | Kwa sababu hiyo, ndugu, tulifarijiwa kwa habari zenu, katika msiba na dhiki yetu yote, kwa imani yenu. |
| 8. | Kwa kuwa sasa twaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika Bwana. |
| 9. | Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha ile yote tunayoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu; |
| 10. | usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuyatengeneza mapungufu ya imani yenu? |
| 11. | Basi Mungu mwenyewe, Baba yetu, na Bwana wetu Yesu, atuongoze njia yetu tufike kwenu. |
| 12. | Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; |
| 13. | apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote. |
| ← 1Thessalonians (3/5) → |