1Samuel (9/31)  

1. Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu.
2. Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote.
3. Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao.
4. Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati ya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata.
5. Hata walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi.
6. Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea.
7. Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, Lakini angalia, kama tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani? Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu wa Mungu; tuna nini sisi?
8. Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama, mkononi mwangu nina robo ya shekeli ya fedha; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha hiyo, atuambie njia yetu.
9. (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.)
10. Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu.
11. Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko?
12. Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu watu wana dhabihu leo katika mahali pa juu;
13. mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hata yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibarikia dhabihu; kisha hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona.
14. Nao wakakwea kwenda mjini; nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli akawatokea, kwenda mahali pa juu.
15. Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema,
16. Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia.
17. Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.
18. Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi?
19. Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako.
20. Na wale punda zako waliopotea siku hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako?
21. Basi Sauli akajibu, akasema, Je! Mimi si Mbenyamini, mtu wa kabila iliyo ndogo kuliko kabila zote za Israeli? Na jamaa yangu nayo si ndogo kuliko jamaa zote za kabila ya Benyamini? Kwa nini basi, kuniambia hivyo?
22. Naye Samweli akamtwaa Sauli na mtumishi wake, akawaleta ndani sebuleni, akawaketisha mahali pa heshima kati ya watu walioalikwa, nao jumla yao walikuwa kama watu thelathini.
23. Samweli akamwambia mpishi, Lete ile sehemu niliyokupa, hiyo niliyokuambia, Iweke akiba.
24. Basi mpishi akatwaa paja, na nyama iliyokuwa juu yake, akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, Iliyowekwa akiba ndiyo hiyo! Iweke mbele yako ule, kwa sababu umewekewa hiyo wewe hata wakati uliokusudiwa, maana nalisema, Nimewaalika watu. Basi Sauli akala pamoja na Samweli siku hiyo.
25. Hata waliposhuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, akaongea na Sauli darini.
26. Nao wakaamka alfajiri; kisha ikawa, kulipopambazuka, Samweli akamwita Sauli darini, akisema, Inuka, nikupeleke kwenu. Basi Sauli akainuka, nao wakatoka wote wawili, yeye na Samweli.
27. Hata walipokuwa wakishuka mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, Mwambie mtumishi atangulie, (naye akatangulia), bali wewe simama hapa sasa, ili nikuambie neno la Mungu.

  1Samuel (9/31)