← 1Samuel (27/31) → |
1. | Ndipo Daudi aliposema moyoni mwake, Siku moja, basi, mimi nitaangamia kwa mkono wa Sauli; hakuna jema zaidi kwangu kuliko kukimbia mpaka nchi ya Wafilisti; naye Sauli atakata tamaa kwa habari yangu, asinitafute tena mipakani mwote mwa Israeli; hivyo nitaokoka katika mikono yake. |
2. | Basi Daudi akaondoka, yeye na hao watu mia sita aliokuwa nao, akamvukia Akishi, mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi. |
3. | Daudi akakaa huko Gathi pamoja na Akishi, yeye na watu wake, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; Daudi naye alikuwa na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, aliyekuwa mkewe Nabali. |
4. | Naye Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia mpaka Gathi; wala hakumtafuta tena. |
5. | Daudi akamwambia Akishi, Sasa kama nimeona kibali machoni pako na nipewe mahali katika miji hii mmojawapo mashambani, nipate kukaa huko; mbona mtumwa wako akae katika mji wa kifalme pamoja na wewe? |
6. | Ndipo Akishi akampa Siklagi siku ile; kwa sababu hiyo huo mji wa Siklagi ni mali ya wafalme wa Yuda hata hivi leo. |
7. | Na hesabu ya siku alizokaa Daudi katika nchi ya Wafilisti ilikuwa mwaka mzima na miezi minne. |
8. | Naye Daudi na watu wake walikuwa wakikwea na kuwashambulia Wageshuri, na Wagirizi, na Waamaleki waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo, tangu Telemu, hapo uendapo Shuri, hata mpaka nchi ya Misri. |
9. | Tena Daudi akaipiga nchi hiyo, asimhifadhi hai mume wala mke, akateka nyara kondoo, na ng'ombe, na punda, na ngamia na mavazi; kisha akarejea na kufika kwa Akishi. |
10. | Naye Akishi humwuliza, Je! Mmeshambulia upande gani leo? Na Daudi husema, Juu ya Negebu ya Yuda, au, juu ya Negebu ya Wayerameeli, au, juu ya Negebu ya Wakeni. |
11. | Tena Daudi hakumhifadhi hai mume wala mke, ili kuwaleta Gathi maana alisema, Wasituchongee kusema, Ndivyo alivyofanya Daudi, tena ndivyo ilivyokuwa desturi yake wakati wote alipokaa katika nchi ya Wafilisti. |
12. | Hivyo Akishi akamsadiki Daudi, akasema, Amewachukiza kabisa hao watu wake Israeli; kwa hiyo atakuwa mtumishi wangu hata milele. |
← 1Samuel (27/31) → |