← 1Samuel (23/31) → |
1. | Kisha wakamwambia Daudi, kusema, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka sakafuni mwa kupuria. |
2. | Basi Daudi akamwuliza Bwana, kusema, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye Bwana akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila. |
3. | Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti? |
4. | Basi Daudi akamwuliza Bwana tena, Naye Bwana akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako. |
5. | Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng'ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila. |
6. | Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake. |
7. | Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo. |
8. | Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumhusuru Daudi na watu wake. |
9. | Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera. |
10. | Ndipo Daudi akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu. |
11. | Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumwa wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumwa wako. Naye Bwana akamjibu, Atashuka. |
12. | Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? Bwana akasema, Watakutia. |
13. | Basi Daudi na watu wake, ambao wapata kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda po pote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akaacha kutoka nje. |
14. | Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake. |
15. | Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi. |
16. | Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu. |
17. | Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa wa pili wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu. |
18. | Na hao wawili wakafanya agano mbele za Bwana; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake. |
19. | Ndipo wale Wazifi wakakwea kwa Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha kwetu ngomeni mwa Horeshi, kilimani pa Hakila upande wa kusini wa Yeshimoni? |
20. | Basi sasa, Ee mfalme, ushuke, kama utakavyo nafsini mwako kushuka; na kazi yetu itakuwa kumtia mkononi mwa mfalme. |
21. | Naye Sauli akasema, Na mbarikiwe ninyi na Bwana; kwa sababu mmenihurumia. |
22. | Nendeni, nawasihi, mkazidi kupata hakika, mkajue na kuona mahali pake anapojificha, tena ni nani aliyemwona huko; maana nimeambiwa ya kwamba atenda kwa hila nyingi. |
23. | Chunguzeni basi, mkayajue maficho yake yote anapojificha; kisha njoni kwangu, tena msikose, nami nitakwenda pamoja nanyi; tena itakuwa, akiwapo katika nchi, mimi nitamtafuta-tafuta katika elfu zote za Yuda. |
24. | Nao wakaondoka, wakaenda Zifu kumtangulia Sauli; lakini Daudi na watu wake walikuwapo nyikani pa Maoni, katika Araba upande wa kusini wa jangwa. |
25. | Basi Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta. Watu wakamwambia Daudi; basi kwa hiyo akashuka mpaka mwambani, akakaa nyikani pa Maoni. Naye Sauli alipopata habari, alimwinda Daudi nyikani pa Maoni. |
26. | Sauli akaenda upande huu wa mlima, na Daudi na watu wake wakaenda upande huu wa mlima; naye Daudi akafanya haraka sana kwenda zake kwa hofu ya Sauli; kwa sababu Sauli na watu wake wakamzunguka Daudi na watu wake ili kuwakamata. |
27. | Lakini akaja mjumbe kwa Sauli, kusema, Njoo upesi, kwa kuwa Wafilisti wameishambulia nchi. |
28. | Basi Sauli akarudi kutoka kumwinda Daudi, akaenda kinyume cha Wafilisti; kwa hiyo wakapaita mahali pale, Selahamalekothi. |
29. | Naye Daudi akakwea kutoka huko, akakaa katika ngome ya Engedi. |
← 1Samuel (23/31) → |