1Samuel (19/31)  

1. Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi.
2. Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha;
3. na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lo lote nitakuambia.
4. Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana.
5. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure?
6. Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa.
7. Basi Yonathani akamwita Daudi, naye Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye alikuwa akihudhuria mbele yake, kama kwanza.
8. Baada ya hayo kulikuwa na vita tena; naye Daudi akatoka, naye akapigana na Wafilisti, naye akawaua kwa uuaji mkuu; nao wakakimbia mbele yake.
9. Tena ikawa, roho mbaya kutoka kwa Bwana ilimjilia Sauli, hapo alipoketi ndani ya nyumba yake, akiwa na mkuki wake mkononi mwake; naye Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake.
10. Sauli akajaribu kumpiga Daudi hata ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule.
11. Kisha Sauli akatuma wajumbe mpaka nyumbani kwa Daudi, ili wamvizie na kumwua asubuhi; naye Mikali, mkewe Daudi, akamwambia, akasema, Wewe usipojiponya nafsi yako usiku huu, kesho utauawa.
12. Basi Mikali akamtelemsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka.
13. Ndipo Mikali akakitwaa kinyago, na kukilaza kitandani, akatia na mto wa singa za mbuzi kichwani pake, na kukifunika kwa nguo.
14. Naye Sauli alipotuma wajumbe ili kumkamata Daudi, yeye alisema, Hawezi.
15. Basi Sauli akawatuma hao wajumbe ili wamtazame Daudi, akisema, Mleteni kwangu juu ya kitanda chake, nipate kumwua.
16. Nao wajumbe walipoingia, kumbe! Kuna kinyago kitandani, na mto wa singa za mbuzi kichwani pake!
17. Sauli akamwambia Mikali, Mbona wewe umenidanganya hivi, na kumwacha adui yangu aende, hata ameniponyoka? Naye Mikali akamjibu Sauli, Yeye aliniambia, Niache niende zangu; kwa nini nikuue?
18. Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwendea Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Sauli aliyomtenda. Kisha yeye na Samweli wakaenda na kukaa katika Nayothi.
19. Naye Sauli akaambiwa, kusema, Angalia, yule Daudi yuko katika Nayothi, huko Rama.
20. Basi Sauli akatuma wajumbe ili kumkamata Daudi; nao hapo walipowaona jamaa ya manabii wakitabiri, na Samweli amesimama kama mkuu wao, roho ya Mungu ikawajilia wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri.
21. Naye Sauli alipoambiwa, alituma wajumbe wengine, wao nao wakatabiri. Naye Sauli akatuma wajumbe tena mara ya tatu, na wao pia wakatabiri.
22. Kisha yeye mwenyewe akaenda Rama, akafika kunako kile kisima kikubwa kilicho huko Seku; akauliza, akasema, Je! Wako wapi Samweli na Daudi? Na mtu mmoja akajibu, Tazama, wako Nayothi, huko Rama.
23. Basi akaenda Nayothi huko Rama, na roho ya Mungu ikamjilia yeye naye, akaendelea mbele, huku anatabiri, mpaka kufika Nayothi huko Rama.
24. Naye akavua nguo zake, akatabiri mbele ya Samweli, akalala uchi mchana kutwa na usiku kucha siku ile. Kwa hiyo watu husema, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

  1Samuel (19/31)