1Samuel (15/31)  

1. Wakati huo Samweli akamwambia Sauli, Bwana alinipeleka nikutie mafuta, uwe mfalme wa watu wake Israeli; basi sasa, isikilize sauti na maneno ya Bwana.
2. Bwana wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri.
3. Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda.
4. Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu.
5. Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni.
6. Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki.
7. Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri.
8. Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga.
9. Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng'ombe, na vinono, na wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa.
10. Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema,
11. Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha.
12. Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali.
13. Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na Bwana, nimeitimiza amri ya Bwana.
14. Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng'ombe ninaousikia?
15. Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa.
16. Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia Bwana usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema.
17. Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli.
18. Kisha Bwana akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia.
19. Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana?
20. Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.
21. Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali.
22. Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.
23. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
24. Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya Bwana, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.
25. Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana.
26. Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.
27. Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.
28. Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.
29. Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute.
30. Akasema, Nimekosa; lakini uniheshimu sasa, nakuomba, mbele ya wazee wa watu wangu, na mbele ya Israeli, rudi pamoja nami, nimwabudu Bwana, Mungu wako.
31. Basi Samweli akarudi na kuandamana na Sauli; naye Sauli akamwabudu Bwana.
32. Ndipo Samweli akasema, Nileteeni hapa Agagi, mfalme wa Waamaleki. Basi Agagi akamwendea kwa utepetevu. Naye Agagi akasema, Bila shaka uchungu wa mauti umeondoka.
33. Lakini Samweli akamjibu, Kama upanga wako ulivyofanya wanawake kufiwa na watoto wao, vivyo hivyo mama yako atafiwa miongoni mwa wanawake. Basi Samweli akamkata Agagi vipande mbele za Bwana huko Gilgali.
34. Na baada ya hayo Samweli akaenda zake kule Rama; naye Sauli akakwea kwenda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli.
35. Wala Samweli hakuenda tena kuonana na Sauli hata siku ya kufa kwake; lakini Samweli alikuwa akimlilia Sauli; naye Bwana akaghairi ya kuwa amemtawaza Sauli awe mfalme juu ya Israeli.

  1Samuel (15/31)