1Kings (6/22)  

1. Ikawa katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya kutoka wana wa Israeli katika nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Sulemani juu ya Israeli, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa pili, akaanza kuijenga nyumba ya Bwana.
2. Nayo nyumba hiyo mfalme Sulemani aliyomjengea Bwana, urefu wake ulikuwa mikono sitini, na upana wake ishirini, na kwenda juu kwake mikono thelathini.
3. Na ukumbi mbele ya hekalu la nyumba, urefu wake ulikuwa mikono ishirini, kadiri ya upana wa nyumba; na upana wake mikono kumi mbele ya nyumba.
4. Akaifanyia nyumba madirisha ya miangaza yenye kimia.
5. Nao ukuta wa nyumba akauzungushia vyumba, kushikamana na kuta za nyumba kote kote, za hekalu na za chumba cha ndani; akafanya vyumba vya mbavuni pande zote.
6. Chumba cha chini kilikuwa mikono mitano upana wake, na chumba cha katikati kilikuwa mikono sita upana wake, na chumba cha tatu kilikuwa mikono saba upana wake; kwa kuwa upande wa nje akaupunguza ukuta wa nyumba pande zote, ili boriti zisishikamane kutani mwa nyumba.
7. Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba.
8. Mlango wa vyumba vya chini ulikuwapo upande wa kuume wa nyumba; mtu hupanda madaraja ya kuzunguka mpaka vyumba vya katikati, na kutoka vile vya katikati mpaka vile vya tatu.
9. Basi ndivyo alivyoijenga nyumba, akaimaliza; akaifunika nyumba kwa boriti na mbao za mwerezi.
10. Akavijenga vyumba mbavuni mwa nyumba yote, kwenda juu kwake kila kimoja kilikuwa mikono mitano; vikaitegemea nyumba kwa boriti za mwerezi.
11. Neno la Bwana likamjia Sulemani, kusema,
12. Katika habari ya nyumba hii unayoijenga, kama ukienda katika sheria zangu, na kuzifanya hukumu zangu, na kuzishika amri zangu zote na kwenda katika hizo; ndipo nitakapolithibitisha neno langu kwako, nililomwambia Daudi baba yako.
13. Nami nitakaa katikati ya wana wa Israeli, wala sitawaacha watu wangu Israeli.
14. Basi Sulemani akaijenga hiyo nyumba akaimaliza.
15. Akazijenga kuta za nyumba ndani kwa mbao za mwerezi; toka sakafu ya nyumba hata boriti za juu, akazifunika ndani kwa mti; akafunika sakafu ya nyumba kwa mbao za mberoshi.
16. Akajenga mikono ishirini pande za nyuma za nyumba toka chini hata juu kwa mbao za mwerezi; naam, ndani akaijengea chumba cha ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu.
17. Nayo nyumba, ndiyo hekalu la mbele, ilikuwa mikono arobaini.
18. Na ndani ya nyumba, mlikuwa na mwerezi ulionakishiwa maboga na maua yaliyofunuka wazi; mlikuwa na mwerezi mahali pote; wala mawe hayakuonekana.
19. Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la agano la Bwana.
20. Na ndani yake chumba hicho cha ndani mlikuwa na nafasi, mikono ishirini urefu, na mikono ishirini upana, na mikono ishirini kwenda juu kwake; akaifunika na dhahabu safi. Akaifunika madhabahu nayo kwa mwerezi.
21. Hivyo Sulemani akaifunika nyumba ndani kwa dhahabu safi. Akaitenga kwa mikufu ya dhahabu mbele ya chumba cha ndani; akapafunika na dhahabu.
22. Akaifunika nyumba yote kwa dhahabu, hata ilipokwisha nyumba yote; tena madhabahu yote iliyokuwa ya chumba cha ndani akaifunika kwa dhahabu.
23. Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi.
24. Na bawa moja la kerubi lilikuwa mikono mitano urefu wake, na bawa la pili la kerubi mikono mitano; mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili.
25. Na kerubi la pili lilikuwa mikono kumi; makerubi yote mawili walikuwa ya cheo kimoja na namna moja.
26. Kwenda juu kwake kerubi moja kulikuwa mikono kumi, na kerubi la pili vivyo.
27. Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi la pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba.
28. Akayafunika makerubi kwa dhahabu.
29. Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje.
30. Na sakafu ya nyumba akaifunika na dhahabu ndani na nje.
31. Akayafanyia maingilio ya chumba cha ndani milango ya mzeituni; kizingiti na miimo ilikuwa ya pande tano.
32. Hivyo akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende.
33. Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni, yenye pande nne;
34. na milango miwili ya mberoshi; mbao mbili za mlango mmoja zilikuwa za kukunjana, na mbao mbili za mlango wa pili za kukunjana.
35. Akanakshi juu yake makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi; akazifunika kwa dhahabu iliyonyoshwa juu ya machoro.
36. Akaijengea behewa ya ndani safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi.
37. Katika mwaka wa nne nyumba ya Bwana ilitiwa msingi, katika mwezi wa Zivu.
38. Hata katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, na sharti zake zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.

  1Kings (6/22)