| ← 1Kings (22/22) |
| 1. | Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli. |
| 2. | Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli. |
| 3. | Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu? |
| 4. | Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi zangu ni kama farasi zako. |
| 5. | Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana. |
| 6. | Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme. |
| 7. | Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa Bwana tena, ili tumwulize yeye? |
| 8. | Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. |
| 9. | Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla. |
| 10. | Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao. |
| 11. | Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, Bwana asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike. |
| 12. | Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme. |
| 13. | Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema. |
| 14. | Mikaya akasema, Kama Bwana aishivyo, neno lile Bwana aniambialo, ndilo nitakalolinena. |
| 15. | Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme. |
| 16. | Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana? |
| 17. | Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. |
| 18. | Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya? |
| 19. | Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto. |
| 20. | Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. |
| 21. | Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. |
| 22. | Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo. |
| 23. | Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako. |
| 24. | Ndipo akakaribia Zedekia, mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Roho ya Bwana alitokaje kwangu ili aseme na wewe? |
| 25. | Mikaya akamwambia, Angalia, utaona siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche. |
| 26. | Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme; |
| 27. | mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni mtu huyu gerezani, mkamlishe kwa chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani. |
| 28. | Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, Bwana hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote. |
| 29. | Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-Gileadi. |
| 30. | Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha, akaingia vitani. |
| 31. | Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru wakuu wa magari yake thelathini na wawili, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake. |
| 32. | Ikawa wakuu wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Huyo ndiye mfalme wa Israeli Wakageuka juu yake ili wapigane naye; naye Yehoshafati akapiga ukelele. |
| 33. | Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate. |
| 34. | Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana. |
| 35. | Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari. |
| 36. | Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake. |
| 37. | Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria. |
| 38. | Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la Bwana alilolinena. |
| 39. | Na mambo yote ya Ahabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na nyumba ya pembe aliyoijenga, na miji yote aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? |
| 40. | Basi Ahabu akalala na baba zake; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake. |
| 41. | Yehoshafati mwana wa Asa alianza kutawala juu ya Yuda, katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli. |
| 42. | Yehoshafati alikuwa mwenye miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi. |
| 43. | Akaiendea njia yote ya Asa babaye; wala hakugeuka, akifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu wakafukiza uvumba katika mahali pa juu. |
| 44. | Yehoshafati akafanya amani na mfalme wa Israeli. |
| 45. | Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, na uthabiti alioufanya, na jinsi alivyopiga vita, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? |
| 46. | Tena mahanithi waliosalia, hao waliosalia siku za Asa baba yake, akawaondoa katika nchi. |
| 47. | Wala hapakuwa na mfalme katika Edomu; naibu alikuwa ndiye mfalme. |
| 48. | Yehoshafati akafanya merikebu za Tarshishi ziende Ofiri kuchukua dhahabu; walakini hazikuenda; kwa maana merikebu zilivunjika huko Esion-geberi. |
| 49. | Ndipo Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, Watumishi wangu na waende pamoja na watumishi wako merikebuni. Lakini Yehoshafati hakukubali. |
| 50. | Basi Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake; na Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake. |
| 51. | Ahazia mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria, katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka miwili juu ya Israeli. |
| 52. | Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akaiendea njia ya babaye, na njia ya mamaye, na njia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli. |
| 53. | Akamtumikia Baali, akamwabudu, akamghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa mfano wa mambo yote aliyoyafanya baba yake. |
| ← 1Kings (22/22) |