← 1Kings (21/22) → |
1. | Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. |
2. | Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. |
3. | Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. |
4. | Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. |
5. | Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? |
6. | Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. |
7. | Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. |
8. | Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. |
9. | Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, |
10. | mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. |
11. | Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. |
12. | Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. |
13. | Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. |
14. | Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. |
15. | Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. |
16. | Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki. |
17. | Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, |
18. | Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. |
19. | Ukamwambie, ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. |
20. | Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa Bwana. |
21. | Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli. |
22. | Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. |
23. | Tena Bwana alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli. |
24. | Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani watamla. |
25. | (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. |
26. | Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.) |
27. | Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. |
28. | Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, |
29. | Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake. |
← 1Kings (21/22) → |