1Kings (20/22)  

1. Basi, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya jeshi lake lote; nao walikuwapo wafalme thelathini na wawili pamoja naye, na farasi, na magari: akakwea akauhusuru Samaria, akaupiga vita.
2. Akatuma wajumbe kwa Ahabu mfalme wa Israeli, mjini, akamwambia, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi.
3. Fedha yako na dhahabu yako ni zangu mimi; na wakezo na wanao, walio wema, ni wangu.
4. Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Ni kama ulivyosema, bwana wangu, mfalme; mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo.
5. Wajumbe wakarudi tena, wakasema, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi, Hakika nimetuma kwako kusema, Fedha yako, na dhahabu yako, na wake zako, na wanao, utanitolea mimi;
6. lakini kesho kama wakati huu nitatuma kwako watumwa wangu, ili watazame-tazame nyumba yako na nyumba za watumwa wako; na itakuwa kila kipendezacho machoni pako
7. Ndipo mfalme wa Israeli, akawaita wazee wote wa nchi, akasema, Angalieni, nawaomba, mwone, kwamba huyu ataka madhara; maana ametuma kwangu kutaka wake zangu na watoto wangu; na fedha yangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.
8. Wakamwambia wazee wote na watu wote, Usisikie, wala usikubali.
9. Kwa hiyo akawaambia wale wajumbe wa Ben-hadadi, Mwambieni bwana wangu mfalme, Kila uliyotuma kumtakia mtumwa wako kwanza, nitafanya, ila neno hili siwezi kulifanya. Basi wajumbe wakaenda zao, wakamrudishia maneno hayo.
10. Ndipo Ben-hadadi akatuma kwake, akasema, Miungu wanifanyie hivi na kuzidi, yakiwa mavumbi ya Samaria yatatosha makonzi ya watu wote walio miguuni pangu.
11. Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Mwambieni, Avaaye asijisifu kama avuaye.
12. Ikawa, Ben-hadadi alipolisikia neno hilo, naye alikuwa akinywa, yeye na wafalme, mabandani, aliwaambia watumwa wake, Jipangeni. Wakajipanga juu ya mji.
13. Na tazama, nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli, akasema, Bwana asema hivi, Je! Umeona makutano haya yote walio wengi? Angalia, nitawatia leo mkononi mwako; nawe utajua ya kuwa ndimi Bwana.
14. Ahabu akanena, Kwa nani? Akasema, Bwana asema hivi, Kwa vijana wa maliwali wa majimbo. Ndipo akanena, Ni nani atakayepanga vita? Naye akajibu, Ni wewe.
15. Ndipo akawaandika vijana wa maliwali wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawaandika watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba.
16. Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia.
17. Wakatoka wale vijana wa maliwali wa majimbo wakitangulia; na Ben-hadadi akatuma watu, nao wakamwambia, Wako watu wametoka katika Samaria.
18. Akasema, Kwamba wametoka kwa amani, wakamateni wa hai; au kwamba wametoka kwa vita, wakamateni wa hai.
19. Basi wakatoka mjini hao vijana wa maliwali wa majimbo, na jeshi nyuma yao.
20. Wakapiga kila mmoja mtu wake; Washami wakakimbia, na Israeli wakawafuatia; Ben-hadadi mfalme wa Shamu akaokoka amepanda farasi, pamoja na wapandao farasi.
21. Mfalme wa Israeli akatoka, akawapiga farasi na magari, akawapiga Washami pigo kubwa.
22. Naye yule nabii akamjia mfalme wa Israeli, akamwambia, Enenda, kusanya nguvu zako, ujue, na kuangalia ufanyavyo; kwa maana mwakani mfalme wa Shamu atakuja juu yako.
23. Basi watumwa wake mfalme wa Shamu wakamwambia, Mungu wao ni mungu wa milima; ndiyo sababu ya kutushinda sisi; lakini na tupigane nao katika nchi tambarare, na hakika tutawashinda wao.
24. Ufanye neno hili; uwaondoe hao wafalme, kila mtu atoke mahali pake, ukaweke majemadari mahali pao.
25. Kisha ujihesabie jeshi, kama jeshi lililokupotea, farasi kwa farasi na gari kwa gari; nasi tutapigana nao katika nchi tambarare, na bila shaka tutawashinda. Akaisikiliza sauti yao, akafanya kama hivyo.
26. Basi ikawa mwakani, Ben-hadadi akawahesabu Washami, akakwea mpaka Afeki ili apigane na Israeli.
27. Wana wa Israeli nao wakahesabiwa, wakapewa vyakula, wakaenda kupigana nao; wakatua wana wa Israeli mbele yao kama vikundi viwili vya wana-mbuzi; bali Washami wakaijaza nchi.
28. Akaja yule mtu wa Mungu, akamwambia mfalme wa Israeli, akasema, Bwana asema hivi, Kwa sababu Washami wamesema, Bwana ni Mungu wa milima wala si Mungu wa nchi tambarare; basi nitawatia makutano haya yote walio wengi mkononi mwako, nanyi mtajua ya kuwa ndimi Bwana.
29. Wakatua kuelekeana muda wa siku saba. Ikawa siku ya saba vikapangwa vita; wana wa Israeli wakawapiga miongoni mwa Washami siku moja watu mia elfu waendao kwa miguu.
30. Lakini waliosalia wakakimbia mpaka Afeki, mjini; na ukuta ukaanguka juu ya watu ishirini na saba elfu waliosalia. Ben-hadadi naye akakimbia, akaingia mjini, katika chumba cha ndani.
31. Watumwa wake wakamwambia, Angalia sasa, tumesikia ya kuwa wafalme wa nyumba ya Israeli ni wafalme wenye rehema; tafadhali, tuvae magunia viunoni, na kamba vichwani, tumtokee mfalme wa Israeli; labda atakuokoa roho yako.
32. Basi wakajifungia magunia viunoni, na kamba vichwani, wakamjia mfalme wa Israeli, wakasema, Mtumwa wako Ben-hadadi asema Roho yangu, nakusihi, iishi. Akasema, Je! Yu hai bado? Ni ndugu yangu yeye.
33. Wale watu wakaangalia sana, wakafanya haraka kulishika neno hilo kama ni nia yake, wakasema, Ndugu yako, Ben-hadadi. Akasema, Haya! Nendeni mkamlete. Ndipo Ben-hadadi akamtokea, naye akampandisha garini.
34. Na Ben-hadadi akamwambia, Miji ile baba yangu aliyomnyang'anya baba yako nitairudisha; nawe utajifanyia njia huko Dameski, kama baba yangu aliyoifanya huko Samaria. Ahabu akasema, Nami nitakuacha kwa mapatano haya. Akafanya mapatano naye, akamwacha.
35. Basi, mtu mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake kwa neno la Bwana, Nipige, nakusihi. Akakataa yule kumpiga.
36. Akamwambia, Kwa sababu hukuisikiliza sauti ya Bwana, angalia, mara ukitoka kwangu simba atakuua. Na mara alipotoka kwake, simba alimwona, akamwua.
37. Ndipo akaona mtu mwingine, akasema, Nipige, nakusihi. Yule mtu akampiga, hata kumpiga na kumtia jeraha.
38. Basi yule nabii akaenda akamngoja mfalme njiani, amejibadilisha kwa kilemba juu ya macho yake.
39. Ikawa mfalme alipopita, alimwita mfalme; akasema, Mtumwa wako aliingia katikati ya pigano; na tazama, mtu mmoja akanigeukia akaniletea mtu, akaniambia, Umlinde mtu huyu; akipotea kwa njia yo yote, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, au utatoa talanta ya fedha.
40. Ikawa mtumishi wako alipokuwa akitenda haya na haya, yule akaenda zake. Mfalme wa Israeli akamwambia, Ndivyo itakavyokuwa hukumu yako; umejihukumu mwenyewe.
41. Akafanya haraka akakiondoa kilemba machoni mwake, mfalme wa Israeli akamtambua kuwa ni mmoja wao manabii.
42. Akamwambia, Bwana asema hivi, Kwa sababu umemwachilia atoke mkononi mwako mtu niliyemweka ili aangamizwe kabisa, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, na watu wako mahali pa watu wake.
43. Mfalme wa Israeli akaenda nyumbani kwake na moyo mzito, mwenye hasira, akaja Samaria.

  1Kings (20/22)