| ← 1John (3/5) → |
| 1. | Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. |
| 2. | Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. |
| 3. | Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu. |
| 4. | Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. |
| 5. | Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. |
| 6. | Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua. |
| 7. | Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; |
| 8. | atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. |
| 9. | Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. |
| 10. | Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake. |
| 11. | Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi; |
| 12. | si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki. |
| 13. | Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia. |
| 14. | Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti. |
| 15. | Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake. |
| 16. | Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. |
| 17. | Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? |
| 18. | Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. |
| 19. | Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, |
| 20. | ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. |
| 21. | Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; |
| 22. | na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. |
| 23. | Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. |
| 24. | Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa. |
| ← 1John (3/5) → |