← 1Corinthians (5/16) → |
1. | Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. |
2. | Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. |
3. | Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo. |
4. | Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu; |
5. | kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu. |
6. | Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? |
7. | Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; |
8. | basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli. |
9. | Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi. |
10. | Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. |
11. | Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye. |
12. | Maana yanihusu nini kuwahukumu wale walio nje? Ninyi hamwahukumu hao walio ndani? |
13. | Lakini hao walio nje Mungu atawahukumu. Ninyi mwondoeni yule mbaya miongoni mwenu. |
← 1Corinthians (5/16) → |