← 1Corinthians (3/16) → |
1. | Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. |
2. | Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, |
3. | kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? |
4. | Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? |
5. | Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. |
6. | Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. |
7. | Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. |
8. | Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. |
9. | Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. |
10. | Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. |
11. | Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. |
12. | Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. |
13. | Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. |
14. | Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. |
15. | Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto. |
16. | Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? |
17. | Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi. |
18. | Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. |
19. | Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao. |
20. | Na tena, Bwana anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni ya ubatili. |
21. | Basi, mtu ye yote na asijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu; |
22. | kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; |
23. | nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu. |
← 1Corinthians (3/16) → |