1Corinthians (15/16)  

1. Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama,
2. na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure.
3. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko;
4. na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko;
5. na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara;
6. baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala;
7. baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote;
8. na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.
9. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu.
10. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.
11. Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.
12. Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu?
13. Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka;
14. tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure.
15. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi.
16. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka.
17. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu.
18. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea.
19. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote.
20. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.
21. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu.
22. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.
23. Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja.
24. Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu.
25. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake.
26. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.
27. Kwa kuwa, Alivitiisha vitu vyote chini ya miguu yake. Lakini atakaposema, Vyote vimetiishwa, ni dhahiri ya kuwa yeye aliyemtiishia vitu vyote hayumo.
28. Basi, vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote.
29. Au je! Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?
30. Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa?
31. Naam, ndugu, kwa huku kujisifu kwangu niliko nako juu yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu, ninakufa kila siku.
32. Ikiwa, kwa jinsi ya kibinadamu, nalipigana na hayawani wakali kule Efeso, nina faida gani? Wasipofufuliwa wafu, na tule, na tunywe, maana kesho tutakufa.
33. Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.
34. Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.
35. Lakini labda mtu atasema, Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani?
36. Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa;
37. nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo;
38. lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake.
39. Nyama yote si nyama moja; ila nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, nyingine ya ndege, nyingine ya samaki.
40. Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali.
41. Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.
42. Kadhalika na kiyama ya watu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika;
43. hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu;
44. hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.
45. Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.
46. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho.
47. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni.
48. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.
49. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.
50. Ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika.
51. Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
52. kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.
53. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.
54. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda.
55. Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?
56. Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.
57. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
58. Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.

  1Corinthians (15/16)