| ← 1Corinthians (13/16) → |
| 1. | Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. |
| 2. | Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. |
| 3. | Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. |
| 4. | Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; |
| 5. | haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; |
| 6. | haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; |
| 7. | huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. |
| 8. | Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. |
| 9. | Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; |
| 10. | lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. |
| 11. | Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. |
| 12. | Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. |
| 13. | Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo. |
| ← 1Corinthians (13/16) → |