| ← 1Corinthians (12/16) → |
| 1. | Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu. |
| 2. | Mwajua ya kuwa mlipokuwa watu wa Mataifa, mlichukuliwa kufuata sanamu zisizonena, kama mlivyoongozwa. |
| 3. | Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. |
| 4. | Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. |
| 5. | Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. |
| 6. | Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. |
| 7. | Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. |
| 8. | Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; |
| 9. | mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; |
| 10. | na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; |
| 11. | lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. |
| 12. | Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. |
| 13. | Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. |
| 14. | Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. |
| 15. | Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? |
| 16. | Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo? |
| 17. | Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa? |
| 18. | Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. |
| 19. | Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? |
| 20. | Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. |
| 21. | Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. |
| 22. | Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. |
| 23. | Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. |
| 24. | Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa; |
| 25. | ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe. |
| 26. | Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. |
| 27. | Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake. |
| 28. | Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. |
| 29. | Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? |
| 30. | Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? |
| 31. | Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora. |
| ← 1Corinthians (12/16) → |