← 1Corinthians (11/16) → |
1. | Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo. |
2. | Basi nawasifu, kwa sababu mmenikumbuka katika mambo yote, nanyi mmeyashika yale mapokeo vile vile kama nilivyowatolea. |
3. | Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu. |
4. | Kila mwanamume, asalipo, au anapohutubu, naye amefunikwa kichwa, yuaaibisha kichwa chake. |
5. | Bali kila mwanamke asalipo, au anapohutubu, bila kufunika kichwa, yuaaibisha kichwa chake; kwa maana ni sawasawa na yule aliyenyolewa. |
6. | Maana mwanamke asipofunikwa na akatwe nywele. Au ikiwa ni aibu mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa, na afunikwe. |
7. | Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunikwa kichwa, kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume. |
8. | Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume. |
9. | Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume. |
10. | Kwa hiyo imempasa mwanamke awe na dalili ya kumilikiwa kichwani, kwa ajili ya malaika. |
11. | Walakini si mwanamke pasipo mwanamume, wala mwanamume pasipo mwanamke, katika Bwana. |
12. | Maana kama mwanamke alitoka katika mwanamume, vile vile mwanamume naye huzaliwa na mwanamke; na vitu vyote asili yake hutoka kwa Mungu. Hukumuni ninyi wenyewe katika nafsi zenu. |
13. | Je! Inapendeza mwanamke amwombe Mungu asipofunikwa kichwa? |
14. | Je! Hayo maumbile yenyewe hayawafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni aibu kwake? |
15. | Lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni fahari kwake. Kwa sababu amepewa zile nywele ndefu ili ziwe badala ya mavazi. |
16. | Lakini mtu ye yote akitaka kuleta fitina, sisi hatuna desturi kama hiyo, wala makanisa ya Mungu. |
17. | Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara. |
18. | Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; |
19. | kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu. |
20. | Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana; |
21. | kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. |
22. | Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo. |
23. | Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, |
24. | naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. |
25. | Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. |
26. | Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. |
27. | Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. |
28. | Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. |
29. | Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. |
30. | Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. |
31. | Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. |
32. | Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia. |
33. | Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojaneni; |
34. | mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani kwake; msipate kukutanika kwa hukumu. Na hayo yaliyosalia nijapo nitayatengeneza. |
← 1Corinthians (11/16) → |